MTENDAJI Mkuu wa Kampuni ya Quality Group, Arif Sheikh,
ametunukiwa Tuzo ya Kiongozi Mkuu-Fahari ya Taifa la India Mwaka 2016.
Sheikh ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Utawala la
Kampuni hiyo kubwa nchini Tanzania, ametukiwa tuzo hiyo juzi (Septemba 3)
mjini Mumbai, India.
Amepata tuzo hiyo iliyotolewa na taasisi ya The Asia One
Global Indian Leader, baada ya kuonyesha uwezo wa hali ya juu katika kubadili
taswira ya sekta ya biashara nchini Tanzania.
Mbali na Sheikh, wengine waliopata tuzo hiyo ni
Mwanzishili wa kampuni ya Dangote - Aliko Dangote, Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya
Pepsi, Indira Nooyi na Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Microsoft, Satya Nadela.
Pia, taasisi hiyo ikawatambua na kuwapa tuzo hiyo, Nita
Ambani, Mshindi wa tuzo ya Nobeli, Prof Amartya Sen, Gautam Singhania na
Raymond Group.
Kwa nini Sheikh?
Akizungumza katika hafla hiyo, Sheikh aliwashukuru
wafanyakazi wenzake wa kampuni ya Quality Group Limited, hususan mtangulizi
wake katika nafasi ya Mtendaji Mkuu wa kampuni hiyo, Yusuf Manji.
“Imekuwa ni heshima kubwa sana kwangu kupata tuzo hii ya
kimataifa. Ingawa mimi ndiye niliyepewa tuzo hiyo, ninaitoa kuwa ni fahari ya
kampuni ninayoiongoza ya Quality Group Limited. Nimefurahi kwamba nimeingia
katika orodha ya watu waliowahi kupata tuzo hiyo ambao nimekuwa nikivutiwa nao
sana.”
Sheikh alisema ametembea na kufanya kazi katika mabara
mbalimbali, lakini kote hajaona kiongozi anayemvutia kama Rais John Magufuli
ambaye ameapa kumuunga mkono katika jitihada zake mbalimbali za kuliletea
maendeleo taifa la Tanzania.
Mashuhuda wasema
Mmoja wa watu waliohudhuria hafla hiyo alitaja
kilichomfanya Sheikh afanikiwe kupata tuzo hiyo kuwa ni uwezo wake wa
kuelimisha wengine kutumia taaluma zao kwa ajili ya kujiletea maendeleo
endelevu.
“Amekuwa akifanya shughuli zake kwa kuwashirikisha
wafanyakazi wenzake na ukiwauliza wafanyakazi wake watakwambia kuwa kufanya
kazi na Sheikh ni ngumu lakini inakusaidia kujifunza,” alisema.
Kwa sasa Sheikh anakuza kipawa chake cha kuendesha
biashara nchini Tanzania kwa kutekeleza miradi kadhaa ukiwamo mradi wa
FastaFasta unaotoa huduma ya usafiri kwa kutumia pikipiki 60,000 na mradi wa
kuendeleza Mji Mkongwe ambao utakapoingia katika hatua ya tatu, utakuwa moja
ya miradi michache inayotoa ajira kwa Watanzania wengi.
Miradi mingine ni Pamoja worlds ambao ni mradi wa kwanza
nchini Tanzania unaotoa huduma ya mtandao kwa Lugha ya Kiswahili, biashara
mtandao na miradi mingine kadhaa katika sekta zinazoendelea kukua nchini humo
ikiwamo sekta ya Elimu, afya, Teknolojia, mauzo ya nje, Magazeti, Kilimo
Biashara na uchimbaji wa madini ambazo kwa pamoja zimeleta faida ya Dola
Bilioni moja za Marekani
“Kwa pamoja miradi hiyo imeifanya Tanzania kuwa ni nchi
yenye fursa nzuri ya kukua kiuchumi, kukuza ajira pamoja na kuwa eneo salama
la uwekezaji wa kimataifa.”
Source: Jambo Leo